
HIVI karibuni niliandika uchambuzi kuhusu January Makamba na kampeni yake ya urais 2015. Kuelekea mwishoni wa uchambuzi, nilisema kwamba "alipaswa angalau kama msomi kujifunza kidogo kutoka kwa mgombea urais mwenzake wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Profesa Mark Mwandosya, ambaye amejitahidi kuandika kwenye kitabu kimoja, mambo muhimu juu ya matatizo mbalimbali ndani ya CCM." Awali naamini Watanzania wengi tu kwa sababu mbalimbali hawakupata kusoma kauli muhimu ya Profesa Mwandosya ya Julai 13, 2014, kuhusu kugombea urais, hivyo ni vyema ninukuu maneno yake: "Kuteuliwa na chama kuwa mgombea urais ni heshima kubwa na kilele cha utumishi ambao mwanachama anaweza kutoa kwa chama na kwa Taifa. “ Itakuwa ni heshima iliyoje kwangu iwapo chama kitaweza kunifikiria na hatimaye kuniteua kufika hapo. Hata hivyo msinitake nivuke daraja hata kabla ya kulifikia..." Sasa nirejee kwenye kitabu cha Profesa Mwandosya. Kupitia kitabu chake kiitwacho 'Sauti ya Umma ni Sauti ya Demokrasia: Mchakato wa Uchaguzi wa CCM, Mkoa wa Mbeya, 2007' na hata katika kitabu cha pili kiitwacho 'Udhibiti wa Huduma za Kiuchumi', amenikumbusha kanuni ya CCM, inayosema kuwa: "Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu wote na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote". Hakika, Profesa Mwandosya anastahili pongezi kwa kujipambanua kuwa ni mwanachama bora wa CCM. Na haya yote aliandika pindi afya yake ikiwa imezorota kweli. Awali kwenye kitabu anatamka maneno mazito kuhusiana na demokrasia. Anasema: "Dhana ninayojaribu kuisisitiza hapa ni kwamba haki na uhuru wa kupiga kura ya kuchagua uwakilishi ni ya msingi sana. Ni kielelezo cha uhuru na utu wa binadamu. Kura, kwa maana hiyo uchaguzi, uwe ndani ya vyama au katika dola, au hata katika jamii kwa jinsi ilivyojipanga, ni jambo muhimu. Ufuasi wake ni kielelezo cha maendeleo ya jamii, uimara wa chama na maendeleo ya taifa. “ Katika ngazi yoyote ile ya uwakilishi inabidi uchaguzi uwe huru, wa haki na usimamiwe kwa ufanisi. Ndipo matokeo yake yanapoheshimika, hayazui mgogoro na yanaimarisha chama, jamii na Taifa...” Nimeona nitumie kumbukumbu zangu za mchakato wa uchaguzi kuelezea yale ambayo, kwa maoni yangu, hakika hayakufuata misingi na taratibu zilizowekwa." Kwa mfuatiliaji yeyote wa siasa nchini, atakumbuka jinsi ambavyo Profesa Mwandosya alikutana na nguvu kubwa wakati anagombea tena nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupitia Mkoa wa Mbeya, mwaka 2007. Na hali hiyo ilimlazimu Profesa Mwandosya wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Ali Mohamed Shein, mkoani Mbeya mwezi Novemba 2006, amweleze kwenye Kamati ya Siasa ya Mkoa kwamba taarifa aliyopokea ya CCM mkoa ni nzuri, ila 'inampa asilimia 95 au 97 ya picha ya mkoa. 'Kazi yangu ni kukupa taarifa ya zile asilimia 3 mpaka 5 zilizobaki'. Na hizo asilimia chache pia zilimfanya amwite pembeni kwa maongezi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, mara tu Makamu wa Rais alipokwenda kupumzika. Profesa Mwandosya alikuwa ana uhakika kwamba Mwakipesile alikuwa anahusika sana na kampeni za uchaguzi wa CCM. Kwa maelezo yake Profesa Mwandosya anasema: "sina tabia ya kumficha mtu au kumsema mtu bila yeye kuwapo. Sipendi fitina wala majungu. Labda malezi na mafunzo kama mwanasayansi na mhandisi yamenifanya niwe hivyo. Marafiki wananiambia hiyo siyo siasa. Wakisema hivyo nawarudisha kwenye ahadi ya mwanachama wa CCM, 'nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko'!" Kwa kweli Profesa Mwandosya anaonyesha jitahadi kubwa kuzingatia misingi ya uongozi wa CCM. Hapo hapo jambo linalonisikitisha ni jinsi ambavyo anahangaika kuonyesha mara kwa mara kwamba katika mizengwe yote dhidi yake, eti Rais Jakaya Kikwete ni msafi! Nikimnukuu sehemu moja anasema: "Kuhusu Rais, hili ni vema likawekwa wazi na kila nilipoulizwa nilifafanua kwamba ulikuwa ni uzushi mtupu kwamba Profesa Mwandosya hatakawi na Rais Kikwete na uongozi wa juu wa Chama au Serikali. “ Kwanza Rais alikuwa ameniteua katika Baraza la Mawaziri. Kwa maana hiyo mimi ni mmoja wa washauri wake wakuu. Rais hahitaji kumweka mtu Mbeya, ashindane na mimi, nishindwe, ili ionekane sifai. Mantiki iko wapi katika hili? “ Kwani kama alivyotumia uwezo wake kumchagua Profesa Mwandosya basi anao uwezo kikatiba kumweka kando bila kungoja uchaguzi wa CCM. “Pili, wanasahau kwamba mwaka 2007 utakuwa ni mwaka wa 20 tangu hawa wawili Rais Kikwete na Profesa Mwandosya walipoanza kufanya kazi pamoja. Tatu, kisiasa msingi wa kufanya hilo walilomzushia Rais ungekuwa kama Profesa angekuwa tishio kisiasa kwake. Hili halina msingi wowote... Lakini vilevile busara ya kawaida haiwezi ikamfanya Rais awachagulie watu wake viongozi anaowataka na sio wanaotakiwa na wananchi." Kuna nukuu ya Kikwete vilevile akikanusha kuhusika na rafu kwa kusema: "Si kweli. Wanalitumia jina langu kwa malengo ya kisiasa". Anahitimisha kwa kusema: "inawezekana kabisa kwamba baadhi ya viongozi walio chini yake walishabikia yaliyokuwa yakifanyika katika uchaguzi wa Mbeya. Kwani watu wanajiuliza, Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu wa CCM, walipata wapi kiburi hicho cha kuendeleza na kusimamia kampeni kinyume cha taratibu, mpaka dakika ya mwisho?" Ni vyema nikawaeleza wasomaji kwamba pamoja na Profesa Mwandosya kusema mwaka 2007 ulikuwa ni mwaka wa 20 tangu waanze kazi pamoja na Kikwete, kutokana na Profesa kuazimwa na Serikali na kuitumikia kama Kamishna wa Nishati na Petroli na baadaye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, ni jambo linaloaminika sana kwa watazamaji makini wa siasa kwamba uhusiano wao wa kikazi ulikuwa tete sana. Na mimi ni mtu ninayeamini mara nyingi usemi kwamba "panapofuka moshi, kuna moto". Vilevile inaaminika kwamba hata miongoni mwa sababu za Profesa Mwandosya kugombea urais mwaka 2005 ulikuwa ni kutokuwa tayari kumwachia Kikwete apete kirahisi... Lakini kama kuwafungua macho, Profesa Mwandosya katika kitabu chake, anammwagia sifa lukuki Dk. Shein, wakati katika hali ya kawaida ilipaswa sifa kama hizo zimwangukie kwanza Kikwete. Na kwa hicho kipindi kirefu cha kufahamiana, alikuwa na mengi ya kusema. Nikinukuu maneno yake juu ya Dk. Shein: "Mh Shein ni mstaarabu sana. Ni kiongozi mtulivu. Kama humfahamu vizuri unaweza ukadhani hapendi kuzungumza. Sivyo. Ni mzungumzaji sana. Ana uwezo mkubwa wa lugha, zote mbili, Kiswahili na Kiingereza. Sina uhakika kuhusu Kiarabu. Ana ujuzi mkubwa wa kiini au viini vya maneno mengi ya Kiswahili na istilahi yake. “ Ilikuwa ni heshima kubwa na bahati kwangu kufanya kazi chini yake kama Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Mazingira. Kuhusu kuzungumza, tofauti na wengi wetu, yeye huzungumza baada ya kufikiri. Wengi wetu huzungumza kwanza na baadaye hufikiria tulisema nini, au maneno tuliyoyasema yana maana gani au yanaleta madhara gani." Sasa katika hili la kusema Rais 'angeweza kumweka kando bila kungoja uchaguzi wa CCM', inaonekana Profesa Mwandosya ana safari ndefu kidogo mpaka aweze kujiita pia Profesa wa Siasa, maana kwenye siasa inaaminika sana, hasa nadhani katika nchi kama za Tanzania ambako tunakuwa na siasa uchwara kama alivyowahi kusema mbunge wa zamani wa Igunga, Rostam Aziz, kwamba ni bora zaidi kuwaweka karibu maadui zako kuliko mbali. Kitendo cha kumwacha Profesa Mwandosya nje ya Baraza la Mawaziri, kungeweza kusababisha gumzo na hata kukosekana kwa kura za Rais mkoani Mbeya. Suala la kumweka mtu kuchuana naye na kumshinda si jambo la kushangaza ili aonekane ni dhaifu nyumbani kwake. Kupona tena ingekuwa kazi kubwa. Nikizingatia jinsi ambavyo Profesa Mwandosya amepitia kwenye misukosuko, natamani kama angekuwa ameachana kabisa na Uwaziri wa Serikali ya Kikwete na kubaki tu kama mbunge. Naamini pia angekuwa na uhuru mpana wa kuzungumzia matatizo ya nchi bila wasiwasi. Isitoshe, tofauti na viongozi wengi, Profesa Mwandosya ni mtu ambaye hakuingia kwenye siasa kwa sababu za kujikimu kimaisha. Anaandika: "Nimepata shida sana kuwaleza watu, na wao wamepata shida kuamini kwamba, kuwa mbunge na kuwa waziri kumenipunguzia sana uwezo wangu wa kifedha na kiuchumi, lakini kumeniongezea sana ari na uwezo wa kuwatumikia wananchi." Kwa ujumla, Profesa Mwandisya ametoa mchango mkubwa sana kupitia maandiko yake. Kwa mfano, ameweza kukabiliana kwa kirefu na tatizo kubwa la makundi ndani ya CCM bila woga. Kwa kifupi anasema: "Makundi au yanayojiita makundi katika Chama chetu ni tofauti kabisa na Chama cha 'Labour' cha Uingereza, Chama ambacho kina uhusiano wa kijadi na CCM. Ni makundi ya ushabiki wa watu. Ni kama zile zinazoitwa 'Fan Club' ambazo vijana wanampenda mpiga muziki au msanii kwa sababu wanampenda.Ni ushabiki zaidi kuliko makundi. Na makundi mengine yanasema waziwazi kwamba wakati wa uchaguzi ni wakati wa 'mavuno'. Sidhani ni busara kuyatukuza hata kuyatambua makundi hayo." Ameweza kufafanua vizuri sana historia ya CCM na kuhitimisha kitabu kwa kusema yafuatayo: "Tunaweza kuyaweka mafundisho ya zoezi tulilopitia mwaka 2007 katika makundi manne kama ifuatavyo: Umuhimu wa ufafanuzi wa itikadi ya Chama; Kuboresha mchakato wa uteuzi na kuomba kura katika uchaguzi ndani ya Chama; Usimamizi wa zoezi la uchaguzi na wajibu wa watendaji wa Chama na Serikali na athari za matumizi makubwa ya fedha bila udhibiti wa kutosha katika uchaguzi ndani ya Chama." Kwa kumalizia, Profesa Mwandosya ni mtu aliyeweka historia ya kutukuka kwenye jimbo lake kwa kuchaguliwa bila kupingwa kwa vipindi vitatu mfululizo. Na kwa upande wa Mkoa wa Mbeya ni 'Mfalme'. Ananikumbusha usemi wa Kiingereza kwamba "Charity begins at home". Haiwezekani kwamba mtu unataka kugombea nafasi ya juu ya utumishi wa umma nchini, lakini nyumbani kwenu hukubaliki kisawasawa. Ni imani yangu ya dhati kwamba hata asipofanikiwa 2015, akigombea kwa mara ya tatu 2020 atashinda. Jambo ambalo siwezi kuacha kulitaja kutokana na unyeti wake sasa hivi ni mchakato wa kupata Katiba Mpya. Profesa Mwandosya katika hili hajaniridhisha kwamba ni kiongozi wa watu kwa maana ya "kuonyesha njia". Hata basi angekemea lugha za kihuni nk. Ni jambo la kuumiza mno kuona kodi za Watanzania waungwana sana zinateketea. Pengine Profesa Mwandosya asingekuwa Waziri, kama ambavyo nilivyokuwa natamani, angeweza kutusaidia katika kipindi hiki cha giza totoro juu ya Katiba na mwenendo mzima ili tutoke tulipokwama. - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/profesa-mwandosya-na-mbio-za-urais#sthash.sPzVvXca.dpuf
0 comments:
Post a Comment