NIMETOA mfano wa jinsi familia za watu makini zinavyoenenda zinapodhamiria kuwekeza katika elimu ya watoto wao. Hata kama ni familia iliyowakutanisha baba na mama waliokuwa wapenda anasa katika ujana wao wa mwanzo (kabla hawajazaa) wanandoa hao watabadilika mara wanapokabiliwa na suala la kuwalea watoto wao na kuwapa kila kitu kitakachowahakikishia malezi bora na maisha ya ufanisi. Hii ina maana kwamba watahakikisha kwamba watoto wanapata mahali pazuri pa kukulia, nyumba safi, malazi mazuri, chakula chenye lishe ya kutosha, kinga dhidi ya maradhi yanayoepukika, upimaji wa afya zao mara kwa mara, na ubora wa tabia utakaowafanya wawe waungwana katika maisha yao. Kisha, elimu. Elimu ni pamoja na malezi mazuri wanayopata watoto katika kaya walimozaliwa, katika jamii walimokulia, kijijini au mtaani na pia shuleni. Shule imekuwa ni wakala wa familia na jamii ya kijiji au mtaa katika shughuli ya kuendeleza elimu ya mtoto pale ambapo wazazi hawawezi tena kuiendeleza katika mipaka ya familia na jamii ya kijiji au mtaa haiwezi tena kuiendeleza katika mipaka yake. Wazazi na wanafamilia wanatimiza wajibu wao hadi kikomo chao. Wanajamii wa kijijini na mtaani nao wanatimiza wajibu wao hadi wanapokomea, na mtoto anakwenda shule ambako jukumu la muendelezo wa elimu na malezi ya mtoto linapokelewa na walimu na watumishi wengine wa asasi hiyo ya elimu. Kuanzia familia, kijiji, mtaa hadi shule na chuo, wote huu ni muendelezo wa shughuli kuu ya kumlea na kumtengeneza mwanajamii atakayekuwa na manufaa kwake yeye mwenyewe, kwa familia yake, kwa kijiji chake au mtaa wake, na kwa taifa zima na hata jamii iliyo pana zaidi ya kimataifa na dunia nzima. Hivyo ndivyo walivyopatikana walimu wenye sifa, wanafalsafa, watumishi wa umma waliotukuka, viongozi walioacha alama zao katika jamii, watetezi wa kila lililo jema na wapinzani wa kila lililo ovu duniani. Wote walipitia hatua hizo nilizoziainisha hapo juu. Tukisoma biografia (simulizi za maisha) za watu kama Mahatma Gandhi, Jawaharlal Nehru, Julius Nyerere, Nelson Mandela, Martin Luther King Jr na wengne, tunapata taswira ya watu waliolelewa kupitia hatua zote hizo hadi kufikia ujana wao wa kufanya yaliyo mema duniani. Muhimu ni kwamba walikuzwa wakifunzwa kuhusu haki, usawa na utu. Matendo yao wakiwa vijana wapevu yalidhihirisha sifa zilizotokana na jinsi walivyokuzwa toka utotoni. (Kwa anayetaka kufuatilia hili, vipo vitabu vingi vya biografia hapa nchini na katika nchi jirani, Ulaya, Marekani na Asia vinavyoonyesha jinsi viongozi wakuu walivyolelewa na kuelimishwa. Sasa hivi hapa nchini, kinapatikana kitabu cha mhadhiri kijana wa Chuo Kikuu cha Edinburgh, Thomas Molony, aliyeandika juu ya maisha ya utoto na ujana wa Julius Nyerere: Nyerere, The Early Years. Molony anaingia kwa undani maridhawa mazingira alimokulia Nyerere, utamaduni uliomlea, mafunzo kutoka kwa mama na wanafamilia wengine, maudhui ya elimu yake ya awali kabisa, na elimu ya baadaye akiwa shule ya sekondari, na kadhalika hadi Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uskochi. Wazazi, ndugu wa karibu, jamii ya kijijini, walimu aliokutana nao shuleni na katika vyuo, vyote vilikuwa ni mtiririko mmoja wa maarifa, ujuzi, elimu na haiba iliyomjenga Kambarage na akawa hivyo alivyokuwa hadi kifo chake). Kinyume chake hujidhihirisha kwa sifa zilizo kinyume kabisa na hizo nilizozitaja. Watoto wengi waliozaliwa na kukuzwa katika familia za wezi na ambao hawakubahatika kunyooshwa na jamii za kijiji au mtaa, wamekulia katika mazingira ya wizi na hatimaye, wakikua, watakuwa ni wezi wakubwa, majambazi na mafisadi, kwa sababu hayo ndiyo malezi waliyoyapata, na hiyo ndiyo elimu waliyoipata. Silika ya wizi itamfanya wakati mwingine aibe mali yake mwenyewe ikiwa amekosa mtu wa kumwibia. Vivyo hivyo kwa mtoto anayezaliwa na kukuzwa katika mazingira ya ugomvi na mizozo katika familia au mtaani na kijijini. Kila palipo na ugomvi ataparukia, na pasipo na ugomvi atautengeneza. Tunaposema kwamba mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, hiyo ndiyo maana yake. Zipo simulizi za kweli za watoto wa binadamu waliolelewa na wanyama kama mbwa-mwitu na nyani, na wakakutwa wakiwa na tabia za hao walezi wao. Kwa hiyo ni muhimu sana kwa malezi ya watoto wa taifa lolote kuandaliwa, kusimamiwa, kuratibiwa na kudhibitiwa ili kwa kiasi kinachowezekana elimu na mafunzo, tabia na mienendo ya watu wa taifa hili viendane na misigano isiwe mikubwa kupindukia kiasi cha kuifanya nchi isiwe na hulka inayotambulika. Niliwahi kuuliza, na hadi sasa nauliza: Hivi ni kitu gani kinachotambulisha utaifa wa Watanzania? Ni ukarimu? Ni upole? Ni utetezi wa wanyonge? Ni uaminifu na ukweli? Ni ubora wa elimu ya watoto wetu? Ni uzalendo unaojenga mapenzi kwa nchi na watu wake? Ni utetezi wa wanyonge na chuki dhidi ya uonevu na unyanyasaji? Au ni ukatili kwa walio dhaifu? Ni uongo, ulaghai, ubabaishaji, uzandiki na unafiki? Ni vigumu kusema na tukijichunguza tutakuta kwamba sifa hizi zote tunazo kwa asilimia fulani. Kuna mambo katika malezi na elimu yetu ambayo, ama kwa kuyafanya ama kwa kutoyafanya, yametuweka mahali ambapo hatuwezi kusema kwa uhakika kwamba sifa yetu kuu ni hii au ni ile. Ni kwamba tunao watu wema na tunao pia watu waovu kwa viwango vinavyokaribiana mno. Kwa jinsi hii huwezi kujua kwa uhakika Mtanzania ni mtu wa aina gani, na hilo si jambo jema. Ningeulizwa leo ni taifa gani ningependa tujenge, ningejibu: Taifa la watu wapenda haki; watu wanaopendana na wanaowapenda watu wengine; watu wanaojali usawa miongoni mwao na kutendeana mema; watu waaminifu na wanaoamini kwamba maendeleo na mafanikio hayana budi kutokana na kazi; watu wanaotetea haki kwa uwezo wao wote; wanaopingana na kila aina ya uonevu na dhuluma; watu wanaoumizwa wakishuhudia maovu yakitendeka, hata kama anayetendewa maovu si mtu wanayemjua; watu wapendao kusema ukweli wakati wote, hasa kama kusema uongo kutasababisha madhara kwa mtu, kundi la watu au jamii. Watu jasiri, wasioogopa kutetea haki kwa kumhofu mtawala au mkwasi; watu walio tayari wakati wote kutetea haki za wanyonge na watu wasio na uwezo….. na sifa nyingine zinazorandana na hizo. Nimejaribu kuonyesha kwamba shule ni muhimili mkuu katika kuhakikisha kwamba watu wa taifa moja wanachangia sifa kadhaa ambazo ndizo zinawatambulisha, mbele ya mcho yao wenyewe na mbele ya macho ya watu wa mataifa mengine. Tukiendelea na mtindo wa kila familia kujichagulia shule watakakosoma watoto wake, tutakuwa tunamomonyoa, kidogo kidogo, hata ule utaifa tuliokuwa tumeanza kuujenga, na hatimaye kuumaliza kabisa. Zipo asasi nyingine muhimu ambazo zinachangia katika kujenga jamii imara, lakini sidhani kwamba zinaweza kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kuliko shule na mfumo mzima wa elimu wanayopata watoto wa taifa lolote. Hatuna budi kukubali kujinyima ili tupate fedha za kuwekeza katika elimu ya watoto wetu. Serikali yetu iache uvivu, iketi na kufikiri kwa kina; ijue mapato yake yanayopotea yanapotelea wapi, kwa sababu gani na kwa manufaa ya nani. Fedha zinazopotea kila mwaka ni fedha ambazo zingeweza kutupeleka mbali kabisa katika elimu, lakini tunaziachia ziende kwa mbinu za kila aina. Aidha, serikali ipunguze mbwembwe zinazosababisha ubadhirifu wa ajabu kiasi kwamba hata hao tunaowaita wahisani wanashangaa ni jinsi gani nchi masikini kama tunavyojitangaza inaweza kuwa na ubadhirifu kama wetu. Hatuna budi kupunguza safari za nje na zinapofanyika iwe ni kwa sababu mahususi na zipunguziwe viwango vya matumizi. Yako mambo mengi ambayo yamo ndani ya uwezo wetu, lakini hatutaki kuyaona kwa sababu ya ulafi mkubwa miongoni mwa watawala wetu na kiwango kikubwa cha kutojali. Au haya yote yanatendeka, au hayatendeki, kwa sababu wahusika hawaoni kama kuna tatizo?

0 comments:

Post a Comment

 
Top