JUMAMOSI iliyopita niliamua kwenda ziarani kulizuru kaburi la Karl Marx, mwanafalsafa wa Kijerumani ambaye fikra zake za kisiasa zimekuwa na athari kubwa katika ulimwengu wa leo.
Marx amezikwa katika kiunga cha makaburi ya mtaa wa Highgate ulio kaskazini mwa London, sio mbali na nyumba ya Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Hiyo haikuwa mara yangu ya kwanza kulizuru kaburi la Marx.  Nimeshawahi kulizuru mara kadhaa, mara zote nikiwapeleka rafiki zangu waliokuwa wakitembea Uingereza.  Kwa hakika, watu kutoka kila pembe ya dunia wamekuwa wakilizuru kaburi la Marx.
Safari hii nilikwenda kwa sababu mimi na mwenzangu mmoja tuliweka nadhiri. Nayo ni kwamba kikishinda chama cha Syriza katika uchaguzi mkuu wa Ugiriki wa Januari 25 tutakwenda kwenye kaburi la Marx kumpigia saluti.
Marx alikuwa na mwenzake, mwanafalsafa wa Kijerumani kama yeye aliyekuwa akiitwa Friedrich Engels.
Wao wawili, wakiwa na midevu yao na misharubu yao, ndio waanzilishi wa nadharia inayojulikana kuwa ni falsafa ya Kimarx. Wote walizaliwa Ujerumani na walifia London.
Marx aliyemzidi umri Engels kwa miaka miwili ndiye aliyefariki mwanzo Machi 14, 1883.  Kwa muda wa miaka 34 kabla hajafariki Marx alikuwa akiishi sehemu za kaskazini mwa London.  Alipolikanyaga jiji la London kwa mara ya mwanzo alikuwa ni mkimbizi wa kisiasa aliyekuwa akisakwa na serikali za takriban nchi zote za Ulaya.
Alipowasili London, Marx alikuwa hohehahe. Engels ndiye aliyekuwa akimsaidia kimaisha.  Akimlisha yeye na familia yake pamoja na wanamapinduzi wengine waliokuwa malofa kama Marx.
Engels ndiye aliyasimamia mazishi ya Marx alipofariki na kugharamia kaburi alimozikiwa katika hicho kiunga cha Highgate.  Kiunga hicho kina sehemu mbili: ya magharibi na ya mashariki. Ya mashariki ndiyo inayojulikana sana kwa sababu huko ndiko alikozikwa Marx.
Baada ya kuanguka kwa Ukomunisti katika nchi za Ulaya ya Mashariki kuanzia 1989, wengi wakifikiri kwamba nadharia ya Umarx itatupwa katika jaa la historia.
Waliokuwa na dhana hizo walikosea, tena walikosea pakubwa. Hii leo fikra za Marx zimeibuka na kuanza tena kuwavutia watu, hususan katika nchi zilizoendelea na za Amerika ya Kusini.
Hata nchini China siku mbili hizi kumekuwa na msisitizo wa kutalii upya itikadi ya Umarx.  Mwishoni mwa Januari hii, Rais Xi Jinping, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, aliwataka wanachama wa chama chake waithamini itikadi hiyo na waitumie kama msingi wa kinadharia wa chama chao.
Xi aliwataka Wakomunisti wenzake wa China waitumie itikadi hiyo kuyatanzua matatizo yao wakati nchi yao inaposonga mbele na mageuzi yake ya kiuchumi.
Katika nchi zilizoendelea nadharia hiyo ya Umarx inafundishwa tena katika vyuo vikuu na vitabu vya Marx na Engels vinauzwa kwa wingi. Vitabu kuhusu nadharia yao pia navyo siku hizi vinaandikwa na kuuzwa kwa wingi kushinda miaka 20 iliyopita.
Kilichozifufua fikra za Marx ni hali ngumu ya uchumi katika nchi zenye ubepari uliopevuka. Wenye kupanga mikakati ya kuokoa uchumi katika nchi hizo wamepigwa na bumbuwazi hawajui nini kilichoukumba mfumo wao wa kibepari.
Kila wanachojaribu kufanya kuukwamua uchumi hakidumu, haichukui muda hushindikana. 
Badala yake wanajikuta wanakabiliwa na matatizo ya kifedha ya aina kwa aina, yakiwa pamoja na mabenki yaliyofilisika na mikopo isiyoweza kulipwa. Mikopo hiyo ni ya watu binafsi na hata ya serikali. 
Ugiriki, kwa mfano, imeelemewa na madeni mengi.  Deni kubwa imekopeshwa na Muungano wa Ulaya ili iweze kulipa madeni, lakini mengi ya madeni hayo ni madeni inayodaiwa Ugiriki na huohuo Muungano wa Ulaya. 
Kwa hivyo, ilichokuwa Ugiriki ikifanya tangu Muungano wa Ulaya utoe mkopo wa kuidhamini nchi hiyo isifilike ni kulipa riba ya madeni inayodaiwa na huo Muungano wa Ulaya.
Hiyo ndiyo hali ya Ugiriki ya leo.  Akhasi zaidi kwa Ugiriki ni kwamba imekuwa haiwezi kufurukuta kwa sababu mikono yake imekuwa kama iliyofungwa minyororo kwa vile mamlaka yake yameporwa na Muungano wa Ulaya.
Hali kama hiyo ya madeni yenye kukaba roho pia iko Uhispania.  Na inaitishia Italia na hata Ufaransa, kwa kiwango fulani.
Uingereza na Marekani yake juu ya utajiri wao nazo zina wananchi wengi wanaoishi kwa taabu.
Idadi ya watu wasioweza kulipa madeni yao inaongezeka kila siku nchini Marekani, Uingereza na kwingine katika bara la Ulaya.  Katika nchi hizo idadi inazidi kuongezeka ya watu wanaotegemea misaada ya chakula cha bure katika yale yaitwayo “mabenki ya chakula.”
Ndio maana kuna migomo, maandamano yasiyokwisha na vilio vya wanaolalamika kuhusu hali zao za kimaisha.
Mimi na mwenzangu tulipoagana kwenda kulizuru kaburi la Marx tuliamua kufanya hivyo kwa sababu ushindi wa chama cha Syriza, chenye kuongozwa na Alexis Tsipras, unaweza ukaibadili sura nzima ya bara la Ulaya na hata kulisaidia bara letu. 
Sababu nyingine ni kwamba Syriza ni chama chenye itikadi ambayo tunatamani pangekuwako chama Tanzania chenye kuifuata.
Chama hiki ni umoja wa vyama kadhaa kama vile ulivyo umoja wa Ukawa Tanzania.  Tofauti kubwa baina ya Syriza na Ukawa ni hiyo ya kiitikadi. Syriza kinafuata itikadi ya mrengo wa kushoto iliyoelemea sana katika Umarx.
Ni chama ambacho viongozi wake wengi ni wasomi.  Baadhi yao ni wahadhiri wa vyuo vikuu, wengine ni maprofesa.  Takriban wote ni wafuasi wa itikadi ya Umarx.
Na ndio maana mimi na mwenzangu tukaagana kwamba chama hicho kitaposhinda uchaguzi tutakwenda kulizuru kaburi la Marx.
Ziara hiyo ilikuwa ni namna ya kumpongeza Marx kwa jinsi fikra zake zilivyowavutia wengi wakakipigia kura chama cha Syriza.
Uchambuzi wa Marx wa mfumo wa ubepari ulikuwa na dosari zake.  Hata hivyo, tukiuangalia uchumi wa dunia ulivyo tunaona kwamba mengi aliyoyatabiri yametokea.  Makampuni, kwa mfano, kwa kutaka faida kubwa siku hizi yanahitaji wafanya kazi wachahe kuliko zamani. Wakati huohuo kunakuwa na umati mkubwa wa walio maskini na wasio na ajira. Tunayaona hayo kwingi, hasa Marekani.
Kwa hivyo, tukitaka pia kumpongeza Marx kwa alivyokuwa akiona mbele. Jinsi alivyotabiri kwamba umaskini daima utakuwa moja ya sababu za kuzuka migogoro katika jamii. Jinsi alivyotambua kwamba mfumo wa kibepari unajichimba wenyewe, kwamba hauwezi kuselelea vivyo ulivyo na kwamba hatimaye umma utanyanyuka na kutafuta mfumo mbadala.
Hivyo ndivyo walivyoanza kufanya Wagiriki waliokipigia kura Syriza wakiamini kwamba chama hicho kitaitanua demokrasia katika jamii.
Wagiriki hao wanataka nchi yao irejeshewe mamlaka yake ya kitaifa kutoka Muungano wa Ulaya.  Dai lao linalingana na lile la Wazanzibari wenye kudai Zanzibar irejeshewe mamlaka yake ya kidola yaliyoporwa na Muungano wa Tanzania.
Jambo lingine la Ugiriki linalofanana na la Tanzania ni ufisadi uliokithiri.  Miongoni mwa mambo yaliyowafanya Wagiriki wengi wakipigie kura Syriza ni msimamo wake dhidi ya ufisadi na dhidi ya sera za kubana matumizi ya serikali.
Hizi sera za kubana matumizi ya serikali ni sera ambazo Ugiriki ilishurutishwa izifuate na Muungano wa Ulaya, Idara ya Mchango wa Fedha za Mataifa (IMF) pamoja na Benki Kuu ya Ulaya.
Matokeo ya sera hizo yalikuwa ni maafa makubwa kwa Wagiriki. Nitoe mfano mmoja tu: nakumbuka nadhani ilikuwa 2012, ambapo bwana mmoja, mfamasia aliyekuwa hana kazi na aliyekuwa hana njia ya kujipatia fedha, alipojiua Athens, mji mkuu wa Ugiriki. 
Kabla ya kujiua aliandika kijibarua akakiacha karibu na alipojiua akieleza kwamba anajiua kwa sababu ya sera za serikali za kubana matumizi.
Aliandika kwamba hakutaka kuanza kujitafutia chakula kwa kuchakura kwenye madebe ya taka. Wala hakutaka kuwa mzigo kwa mwanawe.
Syriza kimeahidi  kwamba hakitozifuata sera hizo za kubana matumizi. Zaidi ya hayo  kinadai Ugiriki isamehewe madeni yake.
Hii leo Ugiriki ni nchi ambayo idadi kubwa ya wakaazi wake, pengine nusu ya vijana wake, hawana ajira.
Lakini kwa sababu ya sera za kubana matumizi serikali haiwezi kuchukua hatua za kuwasaidia. Matokeo yake ni kwamba wengi wao hawana cha kutia mdomoni. Ndio maana maelfu yao, hata wa tabaka la kati la waliosoma, kila siku hupiga foleni mitaani kudoea supu ya bure.
Uingereza nayo ingekuwa na hali kama hiyo.  Tayari kuna “mabenki ya chakula”, mahala ambapo wasio na chakula hupiga foleni kupata vyakula vya bure.  Lakini kuna mambo mawili matatu yanayoisaidia Uingereza isiifikie hali ya Ugiriki.
La kwanza ni kwamba Uingereza ina benki kuu yake yenyewe iliyo huru. Tena inaweza kujipangia na kuitekeleza sera yake ya kiuchumi kwa sababu ina sarafu yake yenyewe.
Mambo hayo yanakosekana Ugiriki. Nchi hiyo, kama ilivyo Zanzibar ndani ya Muungano, inakosa mengi. Haina uhuru kamili wa kujiamulia sera zake, haina sarafu yake yenyewe inayoweza kuisarifu itakavyo na inaambiwa au kushurutishwa nini cha kufanya na wakubwa walio nje ya nchi hiyo.
Kuna msemo maarufu wa Marx ambao umeandikwa kwenye jiwe lililo kwenye kaburi lake. Msemo wenyewe ni huu: “Siku zote wanafalsafa wamekuwa wakiufafanua tu ulimwengu, kwa namna mbalimbali. (Lakini) Lengo liwe ni kuubadili.”
Hivyo ndivyo walivyoanza kufanya viongozi wa Syriza huko Ugiriki na ndivyo Watanzania wengi wanavyotumai kwamba Ukawa nao wataweza kufanya Tanzania.
-

0 comments:

Post a Comment

 
Top