Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia,” hii ni kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2014. Hata hivyo, leo wakati wanawake duniani kote wakisherehekea siku hii muhimu kwao, ni mwaka mmoja mmoja umebakia ili kutimiza malengo ya milenia.
Kukuza usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake ni lengo la tatu kati ya malengo manane ya milenia yaliyowekwa mwaka 1990 na Umoja wa Mataifa UN, huku yakitakiwa kufikiwa kwa mwaka 2015.

Shabaha kubwa ya lengo la tatu ni kuondokana na jinsia tofauti katika elimu ya msingi na sekondari, ikiwezekana ifikapo mwaka 2015, na katika ngazi zote za elimu kabla ya mwaka 2025.

Tangu kuwekwa kwa malengo hayo, dunia imefanikiwa kupata usawa katika elimu ya msingi kati ya wasichana na wavulana, lakini ni nchi mbili pekee nje ya 130 zimekuwa na mafanikio katika kutimiza lengo  katika ngazi zote za elimu.
Kimataifa, wanawake 40 kati ya 100 waliweza kufanya kazi nyingine tofauti na kazi za kilimo mpaka kufikia mwaka 2011. Hili lilianza kuboreshwa tangu mwaka 1990.

Katika nchi nyingi, suala la usawa wa kijinsia limeendelea kufanyiwa kampeni, lakini bado wanawake wengi wanaendelea kukabiliwa na ubaguzi, katika upatikanaji wa elimu, kazi na mali za kiuchumi na kushirikishwa katika maamuzi na uongozi serikalini.

Kwa mfano katika kila nchi inayoendelea wanawake wameonekana kushikilia na kufanya vizuri katika kila kazi au nyadhifa wanazoshikilia ukilinganisha na wanaume, huku wakifanya mambo yenye faida na maendeleo kwa jamii.

Wakati haya yakifanikiwa, ukatili dhidi ya wanawake, unaendelea kuzorotesha jitihada za kufikia malengo yaliyowekwa.
Hata hivyo, umaskini umekuwa kikwazo kikubwa, kilichosababisha kushindwa kujiunga na shule za sekondari, hasa miongoni mwa wasichana wakubwa.

Wanawake wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na mazingira magumu ya ajira, hasa maeneo ya ofisi na kazi nyingine za kuajiriwa.

Mafanikio ya malengo Tanzania

Tanzania imefanikiwa kwa kiasi katika malengo haya. Kwa upande wa elimu imefanikiwa kuhakikisha idadi kubwa ya wasichana wanakwenda shule hasa za msingi. Hata hivyo sekondari za kata umekuwa mkombozi mkubwa kwa wanafunzi wa kike waliomaliza elimu ya msingi na kukosa shule za kuendelea na masomo hasa vijijini
Miaka mitano nyuma, ilikuwa kawaida kwa msichana kuolewa pindi anapomaliza elimu ya msingi. Hivi sasa ni nadra, wengi wao wamekuwa wakijiunga na masomo ya sekondari katika shule mbalimbali zilizopo maeneo ya jirani na vijiji wanavyoishi.

Hata hivyo, elimu ya juu imeboreshwa sambamba na ufaulu wa masomo ya sayansi kwa wasichana, huku kukiwa na shule kadhaa za wasichana pekee, ambazo zimeweza kufanya vizuri. Kwa miaka mitatu mfululizo, wasichana wamekuwa wakifanya vizuri kidato cha nne na sita, huku matokeo ya mwaka huu kati ya 10 bora kulikuwa na wasichana saba.

Hata hivyo, kumekuwa na mikakati ya kuhamasisha wanafunzi wa kike kupendelea somo la hesabu, huku motisha mbalimbali zikitolewa ili kuwafanya wapendelee zaidi. Mafanikio ni makubwa kwani kumeweza kuwa na wanawake wengi, wanaofanya kazi zinazohusu usimamizi wa fedha.

Suala la pili ilikuwa ni kuwawezesha wanawake. Katika hili Tanzania imefanikiwa kwa asilimia kubwa, kwani imeweza kuanzisha mikopo mbalimbali inayowahusu wanawake ikiwemo Vikoba, Mkukuta, Mkurabita, Pride na nyinginezo. Kwa upande wa kuwekeza, zimeanzishwa benki za wanawake ambazo zimekuwa zikiwahamasisha wajasiliamali na wafanyakazi kuwekeza.
Mikopo hiyo imewawezesha wanawake wajasiriamali kufanya biashara na kufungua viwanda mbalimbali,  wengi wameweza kuchangia uchumi wa kaya, kusomesha watoto na kufanya shughuli  za kijamii.

Kumekuwa na idadi kubwa ya wanawake ambao wamefanikiwa kukamata nyadhifa kubwa, katika nafasi za juu kwenye ofisi, kampuni na hata serikalini. Idadi ya wanawake wanaowakilisha katika siasa ni ya kuridhisha huku wakipewa nyadhifa za juu.

Lengo la tatu ilikuwa ni kukuza usawa wa kijinsia. Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika hili, kwani imeweza kuanzisha dawati maalumu la jinsia katika kila kituo cha polisi, ili kukabiliana na tatizo la unyanyasaji wa kijinsia.
Pia kuwepo kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, kumeweza kufanya kazi nyingi, zilizotoa matokeo chanya katika malengo haya makubwa matatu. Imeweza kupambana na ukatili kwa wanawake, baada ya kutoa elimu kwa jamii sambamba na kuweka vifungu vya sheria, vinavyowabana wanaume wanyanyasaji na wabakaji, kwa kufungwa miaka 30 jela iwapo watakutwa na tuhuma za kubaka.

Madhumuni ya maadhimisho

Madhumuni ya maadhimisho haya ni kutoa fursa ya kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba ya kimataifa, kikanda na kitaifa inayohusu masuala ya maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia.

Madhumuni mahususi ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii, juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa wanawake katika kuchangia na kuleta maendeleo yao endelevu, kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau, katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii, ili waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao, familia zao na taifa kwa ujumla.

Kama kaulimbiu ya mwaka isemavyo ”Chochea Mabadiliko Kuleta Usawa wa Kijinsia,” ujumbe huu unasisitiza kuhamasisha na kuelimisha jamii, kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo
Mwelekeo wa maendeleo  kijamii, kitaifa na kimataifa unasisitiza na kuhimiza kuandaa na kutekeleza mipango inayozingatia ushirikishwaji na ushiriki stahiki wa wanawake na wanaume katika kujiletea maendeleo yao. 

Maadhimisho hutoa fursa maalumu kwa taifa, mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa katika kumwendeleza mwanamke na kubainisha changamoto, zinazowakwamisha kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto  hizo

src
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Top