Dunia hii leo inasherekea Sikukuu ya Wanawake, ambayo huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu ni Chochea Mabadiliko, Kuleta Usawa wa Kijinsia.

Shabaha ya sherehe hizi ambazo huadhimishwa na mataifa mbalimbali duniani, ni kuufahamu na kutambua mchango alionao, anaoutoa mwanamke katika jamii.

Wakati dunia ikiazimisha sherehe hizi leo, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinaikabili jamii hasa ya Afrika katika kulinda haki za mwanamke na kumuweka mbali na kudidimizwa, kukandamizwa na kunyonywa.

Miongoni mwa vitu ambavyo wanawake wa Umoja wa Mataifa, wanaharakati bado wana kazi kubwa ya kulipiga vita, ni baadhi ya makabila kuendelea na mila kandamizi kwa wanawake kama kukeketa watoto wa kike, kuwalazimisha kuzalia nyumbani kwa madai ni ujasiri, kuwanyima haki ya kupata elimu kwa kuona ni hasara
Katika kulitambua hilo Mwananchi Jumamosi lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Helen Kijo-Bisimba, aizungumzie siku hii, kwa kuwa ni miongoni mwa wanawake wanaotetea haki zao.

Dk Bisimba anaanza kusema kuwa kwa mwaka huu, wanawake wana mambo ya kujivunia na ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.

Anasema Tanzania imepiga hatua ukilinganisha na mwaka 1961, ambapo nchi ilikuwa imepata uhuru, mambo mengi yamebadilika, ikiwamo mafanikio katika nyanja ya siasa ambapo wanawake wameingia kwa asilimia 30.

Mila na desturi

Anasema shida kubwa bado ipo kwenye mila na desturi bado ni kandamizi, matukio kama wanawake kubakwa, kupigwa, kudhurumiwa mali bado ni mengi na sheria inashindwa kuchukua mkondo wake kwa kuwa bado kuna mambo ya kujuana.

“Wanawake wengi wanaumizwa na wanaume zao au wanaoishi nao, lakini taarifa zikifika polisi, wanafamilia kwa sababu ya kufahamiana wanataka wakayamalize nyumbani, hali hii inawapa nafasi wana familia kuendelea kuwabana wanawake kwa kuwa wanaelewa hakuna kitakachofanyika,” anasema Dk Bisimba na kuongeza:Nimewahi kusikia wanawake wengi wamenusurika kuuawa, baada ya kupigwa na waume zao na familia kuamua warudi huko huko kwa waume zao  kwa kuwa wao ni wake za watu, wakifika huko wanapigwa mara mbili ya mwanzo, lakini familia bado inakuwa na msimamo uleule wa kuwarudisha,” anasema Dk Bisimba.
Akizungumzia sekta ya afya, Dk Bisimba anasema kuwa kwa upande wa vifo vya watoto kuna mafanikio kiasi kwa kuwa vimepungua, lakini vifo vya mama bado ni tatizo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi, hasa katika suala la miundombinu, huduma za afya  kuwa mbali na jamii, vifaa vinavyotumika kuhudumia wanawake
“Serikali imejitahidi kupunguza vifo vya watoto wachanga, lakini vifo vya kina mama hasa wajawazito bado inatakiwa suala hilo  lifanyiwe kuhakikisha wanawanusuru,” anasema Dk Bisimba.

Anasema katika Nyanja ya elimu kwa mtoto wa kike, kuna changamoto ambayo inaanza baada ya kumaliza darasa la saba, kwani wanapoanza ni sawa kwa sawa kati ya wanaume na wanawake, lakini wakifika mbele wanawake wanarudi nyuma.

Anazitaja sababu ambazo bado wanawake kwa kushirikiana na Serikali na asasi binafsi inabidi wapambane nalo ni mimba za utotoni, ndoa za utotoni, umbali wa shule, mazingira wanayosomea na utamaduni kandamizi.

“Haya ndiyo maeneo mzigo kwa watoto wa kike kama siyo mwanamke kwa ujumla, yakifanyiwa kazi baada ya muda kutakuwa na wanawake wasiokuwa na matatizo na waelewa, wasiohitaji kusaidiwa katika mambo yao,” anasema Dk Bisimba.
Ushirikishwaji Katiba Mpya

Anasema katika Katiba Mpya wanawake wameshirikishwa kwa kiasi fulani, tofauti na hapo mwanzo wakati mchakato unaanza wengi hawakupata nafasi kutokana na wengi wao kuwa na majukumu ya kuangalia familia.

“Katika Bunge Maalumu la Katiba, katika kundi la watu kutoka katika asasi zisizo za kiserikali kati ya 201, 100 ni wanawake, hiyo kwa kiasi fulani inatia moyo na kuona ni kwa jinsi gani mchango wao umethaminiwa,” anasema Dk Bisimba.

Anafafanua kwa wingi huo kama watasimama na kutambua walichotumwa na wanawake wenzao, kuna kila hali ya kumuinua mwanamke, kwa kutambua haki zao nyingi katika Katiba Mpya.

Dk Bisimba anashauri ili kupiga hatua na kusahau shida zote ambazo zinamwelemea mwanamke, ni Serikali kujali elimu yao kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anahitimu masomo yake bila kubagua jinsia, wazazi watilie maanani suala zima la elimu, kwa kuhakikisha kila mtoto anasoma kwa kiwango stahiki, Serikali ijitahidi kuwapunguzia wazazi mzigo wa kusomesha, kwa kuweka mazingira rafiki na rahisi ya elimu.

“Kuna wazazi wanawaambia watoto wao wasifaulu na wakifanya hivyo  watawaanyoosha, wanapinga wasifaulu ili kukwepa gharama za kusomesha wakiwaza malaki mamilioni wanayotakiwa kutoa mtoto akifaulu hasa wa kike wanaona bora aolewe,” anasema Bisimba.
Anaeleza kuwa kama kaulimbiu ya mwaka huu inavyosema kuwa ‘hamasisha mabadiliko’, mabadiliko yanatakiwa kuanzia kwa wanawake na siyo kwa mtu mwingine.

“Wazazi na walimu wahakikishe wanawaeleza umuhimu wa elimu watoto wa kike, huku wakiwatolea mfano wanawake waliofanikiwa, ili kukuza kizazi cha wanawake wasomi na wenye malengo hapo baadaye, wanaoweza kusimamia haki zao, na za wengine,” anasema

src
mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Top