Profesa Palamagamba Kabudi

Profesa Kabudi yu sahihi alichosema Zanzibar
WIKI iliyopita Profesa Palamagamba Kabudi – mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Katiba, alitoa kauli huko Zanzibar inayofikirisha.
Ni kauli inayogusa jambo ambalo limekuwa likinitatiza kwa muda mrefu kupata jibu; maana kila ninapotafakari kulikoni naishia kujiuliza swali lile lile:
Ni werevu wa chama tawala CCM au ni ujinga wa Watanzania?
Akizungumza katika kongamano la kujadili Miaka 50 ya Muungano, Profesa Kabudi aligusia kuhusu kinachoendelea kwenye Bunge la Katiba mjini Dodoma.
 Profesa Kabudi, miongoni mwa mambo mengine mazito yaliyosababisha hata TBC 1 imkatie matangazo, alisema hivi kuhusu suala la shinikizo linaloendelea la kukubaliwa kwa mfumo wa serikali mbili kinyume cha matakwa ya wananchi ya mfumo wa serikali tatu:
“Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wako kwa sababu wewe ujinga wako ndiyo amali yako lakini kwa wengine siyo amali.”

Maneno hayo ya Profesa Kabudi kuhusu ujinga wa kizazi chetu hiki yalinikumbusha kauli nyingine iliyopata kutolewa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ya kwamba Watanzania ni wavivu wa kufikiri.
Mara nyingi (kama sio zote) mjinga ndiye huwa mvivu wa kufikiri. Kwa hiyo, kauli hizo mbili – ya Profesa Kabudi na ya Rais mstaafu Mkapa zinafanana kwa namna fulani.  Zinafanana; maana zote zinazungumzia ujinga na uvivu wa kufikiri wa kizazi hiki cha Watanzania!
Huko nyuma nilipokuwa nikitafakari mustakabali wa taifa letu, niliishia kwenye swali lile lile: Ni werevu wa chama tawala CCM au kweli ni ujinga wa Watanzania unaotokana na uvivu wao wa kufikiri?
Vyovyote vile, sasa naamini pasipo shaka yoyote kwamba, Watanzania tu wavivu wa kufikiri, na kwa sababu tu wavivu wa kufikiri, tu wajinga! Vinginevyo, mambo yasingeenenda katika nchi yetu kama yanavyoenenda, na bado mambo yakaendelea kubaki sawa tu kama yalivyo.
Chukulia mfano wa Bunge la Katiba linaloendelea na kikao chake mjini Dodoma. Watu wengi tu – wasomi na wasio wasomi wamezungumza na wameandika tena na tena na tena ya kwamba, kinachofanyika huko, hivi sasa, ni kutengeneza Katiba ya nchi inayotokana na maoni na msimamo wa CCM, na si wa wananchi.
Wameandika na kuzungumza tena na tena ya kwamba, huwezi kuyaweka pembeni maoni ya wananchi kwenye Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Katiba kwa kuwahoji wananchi sehemu mbalimbali nchini, na kisha ukaibuka na Katiba utakayoiita  “ni ya wananchi”.
Hiyo ni hadaa. Ni hadaa kwa sababu Katiba ya wananchi haiwezi kutengenezwa na chama kimoja tu cha siasa. Ni hadaa kwa sababu Bunge la Katiba limesheheni wajumbe wa CCM tu, na mbaya zaidi wajumbe hao wameamua kuyatosa pembeni maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa kwenye rasimu.
Lakini kwa sababu ya ujinga wetu huo, sisi wananchi wa kawaida hatuioni hiyo kuwa ni hadaa. Maana, kama Watanzania tungekuwa ni werevu na si wajinga, tungalimshinikiza Rais Kikwete kusitisha Bunge hilo la Katiba na kuyaokoa mabilioni ya fedha za walipakodi yanayoteketea bure.
Kwa mtazamo wangu, ni mabilioni  ya pesa za walipakodi yanayoteketea bure kwa sababu, mwisho wa yote, Katiba itakayotengenezwa Dodoma katika mazingira hayo, kamwe haiwezi kuwa ni Katiba ya wananchi. Na kwa maana hiyo, haiwezi kudumu hata miaka 20 tu kabla haijatupiliwa mbali.
Kwa hakika, naweza kwenda mbali zaidi na kusema ya kuwa ingalikuwa ni katika nchi nyingine zenye demokrasia iliyokomaa na wananchi wasio wavivu wa kufikiri na wabunge wasioweka mbele maslahi yao binafsi, Rais Kikwete angelikwishapigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, kwa sababu ya kushindwa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano aliyoapa kuilinda wakati akiapishwa urais.
Lakini kwa sababu ya uvivu wetu wa kufikiri, hatuelewi au hatujui ya kwamba Rais Kikwete ameikosea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukaa kimya na kuiruhusu Zanzibar kuifanyia marekebisho Katiba yake mwaka 2010 – marekebisho ambayo yamepora mamlaka ya Rais wa Muungano (mamlaka yake), na kumfanya asiwe na nguvu zozote Zanzibar.
Kama tungekuwa si wavivu wa kufikiri (wajinga), tungelikwishadai maelezo kutoka kwa Rais Kikwete kuhusu hilo. Tungalikwishamuuliza: Alikuwa wapi mwaka 2010 wakati Zanzibar ikirekebisha Katiba na kuweka vifungu vinavyokiuka Katiba ya Muungano?
Miaka 30 iliyopita aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri, Aboud Jumbe, alishinikizwa na kikao maalumu cha NEC ya CCM, mjini Dodoma, kuachia nyadhifa zake zote kwa kosa kama hilo la Kikwete la kuudhoofisha Muungano.
Nilikuwepo mjini Dodoma mwaka huo wa 1984 nikiwa ripota wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo kuripoti habari za kikao hicho maalumu cha NEC ya CCM, na hivyo nafahamu mjadala uliendaje hadi Mzee Jumbe kung’olewa nyadhifa zake zote.
Katika hicho kilichoitwa “kuchafua hali ya hewa ya kisiasa”, maskini Mzee Jumbe wala yeye hakufikia hatua ya kubadilisha Katiba ya Zanzibar kama alivyoanya Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk. Shein mwaka 2010 kwa “baraka” za Rais Kikwete, lakini bado mzee wa watu alikwenda na maji kwa kudai serikali tatu!
Leo hii, si Dk. Shein wala Kikwete ambao wamehojiwa na NEC ya CCM kuhusu mabadiliko hayo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 yenye vifungu vinavyodhoofisha Muungano.
Lakini hata sisi ambao si wana CCM, kwa ujinga na uelewa wetu mdogo, hatudai maelezo hayo kutoka kwa Rais wetu Kikwete na kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein.
Na mbaya zaidi, tunaukubali kirahisi uamuzi wao mwingine na wa chama chao cha CCM wa kuyatosa maoni ya wananchi katika rasimu ya Katiba yanayotaka muundo wa serikali tatu, na tunakubali kushinikizwa muundo wa serikali mbili kinyume na matakwa yetu wananchi.
Katika hoja yake ambayo ameirudia hivi karibuni, Rais Kikwete anadai ya kuwa idadi ya waliohojiwa na Tume ya Warioba haihalalishi kuhitimisha kuwa Watanzania wengi wanataka muundo wa serikali tatu.
Kwa maneno mengine, anaupigia debe mfumo wa serikali mbili ambao wala wananchi hawakuwahi kuhojiwa kama ndio wanaoupenda – mfumo ambao umekuwa ukilalamikiwa kote nchini, na hasa Zanzibar kwa karibu miaka 40 sasa!
Lakini hata kama Rais Kikwete ana hoja nzito kwamba Tume ya Warioba haikuhoji wananchi wengi, na hivyo haina haki ya kusema kuwa Watanzania wengi wanataka mfumo wa serikali tatu, bado busara si kushinikiza Bunge la Katiba liukubali mfumo wa serikali mbili.
Kwa mtazamo wangu, busara ingekuwa ni kuirejesha tena kazini tume hiyo ya Warioba na kuipa muda zaidi wa kuwahoji wananchi wengi zaidi (idadi yoyote ile anayoona yeye inatosha), lakini si kushinikiza Bunge la Katiba liukubali mfumo wa serikali mbili, na wala si kuikejeli rasimu hiyo na maoni hayo ya wananchi wanaotaka serikali tatu kama anavyofanya sasa.
Huko nyuma, Jenerali Ulimwengu alipata kuandika ya kwamba Katiba si jambo la haraka haraka, na kwamba tunaweza kuiandaa hata kwa miaka mitano.
Aliandika pia ya kwamba yale mapungufu tuliyonayo (mathalan kutokuwepo kwa tume huru ya uchaguzi) ambayo yanahitaji kutatuliwa haraka, yanaweza kushughulikiwa kwa njia za kawaida kama vile kutungiwa sheria nk; huku wakati huo huo tukiendelea na mchakato wetu wa muda mrefu wa kuandaa Katiba imara ya nchi itakayodumua miaka 100 na zaidi!
Nakubaliana naye (Jenerali) kabisa. Hakuna uharaka wowote katika kuandaa Katiba imara. Hakuna u-fastafasta katika kuandaa Katiba ya nchi.
Na ikizingatiwa utata na maajabu yaliyojitokeza mpaka sasa ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu kutoswa pembeni, sioni mantiki ya kikao hicho cha Bunge la Katiba, mjini Dodoma,  kuachwa kiendelee. Kufanya hivyo, ni kuteketeza bure mabilioni ya pesa za walipakodi nchini.
Mantiki ninayoiona mimi ni ya kurudi nyuma – yaani mchakato uanze upya; hata kama utatuchukua miaka mingine mitano kuukamilisha.
Na tena mchakato huo ukianza upya uanzie kwenye kuirekebisha Sheria yenyewe ya Mabadiliko ya Katiba – sheria  ambayo, kama sote tunavyofahamu, inampa rais mamlaka makubwa isivyo lazima na isivyo haki.
Lakini ni nani wa kumshinikiza Rais Kikwete aione mantiki hiyo ya kuvunja kikao hicho cha Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma?
Ni hawa Watanzania walio wavivu wa kufikiri, na ambao kwao mijadala kuhusu mechi za Yanga na Simba au Manchester na Chelsea ina maana kubwa kwao kuliko suala la Katiba mpya ya nchi yao?
Vyovyote vile, Rais Kikwete na CCM yake wanaweza kutumia ujinga huo wa wananchi na hatimaye kutengeneza Katiba wanayoitaka wao. Hata hivyo, tumkumbushe kwamba Katiba ya namna hiyo haitadumu miaka mingi kabla ya kutoswa; maana ujinga wa Watanzania wa leo siyo ujinga wa Watanzania wa kesho!
Nihitimishe kwa kurudia kusema ya kwamba Profesa Kabudi yu sahihi kabisa kwa tahadhari yake ile aliyoitoa Zanzibar juu ya upuuzaji huo wa maoni ya wananchi kuhusu aina ya Muungano wanaoutaka. Profesa yu sahihi alipotahadharisha
“Ujinga wa kizazi hiki tusidhani utakuwa ujinga wa kizazi cha kesho. Vizazi vijavyo vya Tanzania vitakuwa na ujinga wake. Ni vyema kuwawekea misingi lakini waje kuishi na ujinga wao kuliko kulazimisha ujinga wetu, kwa sababu ujinga wetu ndiyo amali yetu lakini kwa wengine siyo amali”!

src
Raia mwema

 

0 comments:

Post a Comment

 
Top