BAJETI ya Serikali imepita jana baada ya kuridhiwa na wabunge wengi wakiwemo baadhi ya Kambi ya Upinzani, ambapo Wabunge waliopiga kura za Ndiyo 234, Hapana 66.
Bajeti hiyo ilipitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho kwa kukata fedha kwenye matumizi ya kawaida na kupata Sh bilioni 165.82 zilizopelekwa kwenye mahitaji zaidi.
Maeneo yaliyonufaika na mabadiliko hayo ni Jeshi la Zimamoto, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Mengine ni Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Uchukuzi, Idara ya Uhamiaji na Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Wizara ya Ajira.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mbunge wa Magu, Dk Festus Limbu (CCM), aliwasilisha taarifa ya mashauriano ya Kamati hiyo na Serikali jana bungeni, iliyoonesha maeneo yaliyoongezwa fedha.
Dk Limbu alisema katika mashauriano hayo, walikubaliana kukata matumizi ya kawaida na kupata Sh bilioni 165.82, ambazo zilipelekwa katika maeneo yaliyoonekana kuwa na mahitaji zaidi, na kati ya hizo Sh bilioni 34, zilienda katika maendeleo.
Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum, alielezea kuwa kodi ya mishahara itaendelea kupunguzwa katika bajeti ijayo na katika bajeti ya sasa kiwango kilichopunguzwa ni kile kile cha asilimia moja, kutoka asilimia 13 mwaka uliopita wa fedha mpaka asilimia 12 mwaka huu wa fedha.
Hata hivyo alisema wakati wafanyakazi wametetewa na wabunge kwa hoja nzito wasipunguziwe kodi bila kuomba na kushawishi, wafanyabiashara hawataki kulipa kodi ndio maana alipotangaza vyanzo vya mapato, wote walijazana Dodoma.
Waziri Mkuya alisema ametumiwa ujumbe wa simu akiambiwa asiende kufuta kodi kwa kuwa ataaibika na kusema, yuko tayari kupigania hatua hiyo ili kodi ilipwe.
Aliwataka wabunge kumuunga mkono wakati wa kufuta misamaha ya kodi na kupambana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali yaliyopo mpaka katika halmashauri.
Alitoa mfano wa madeni yaliyowahi kuwasilishwa Hazina ya Sh trilioni 1.5, walipofanya uhakiki wakakuta madai halisi ni Sh bilioni 150.
Pia, alitoa mfano wa mmoja wa watumishi ambaye madai yake yalionesha ni Sh milioni 600, lakini alipoulizwa mwenyewe akashangaa na kutoa risiti zilizoonesha kuwa anadai Sh 600,000 tu.
Aliwaomba wabunge wamuunge mkono wakati wa kutengeneza sheria ili watumishi wa Serikali wasio waaminifu, wachukuliwe hatua kali za kisheria

0 comments:

Post a Comment

 
Top