KATIKA makala yangu ya mwisho niliandika kwamba ni sisi wenyewe tutakaoisalimisha nchi yetu na sisi wenyewe tutakaoizamisha katika majanga. Yote haya yatategemea jinsi tunavyotenda mambo yetu katika nyanja mbalimbali.
Huu ni ukweli usiohitaji ubishi mrefu. Kila jamii hupata sudi iliyoifanyia kazi. Jamii ya watu wavivu sudi yake ni kubaki nyuma kimaendeleo na hata kufa njaa. Jamii ya watu wagomvi sudi yake ni vita za kila mara na mapigano yasiyoisha. Jamii ya watu wachoyo sudi yake ni kunyang’anyana daima, hata pale inapokuwa na rasilimali nyingi.
Kinyume cha sifa hizi mbaya ni jamii ya watu waongofu, wenye mshikamano na wanaogawana kwa haki hata pale wanapokuwa na rasilimali kidogo.Sote tumeshuhudia ukweli wa haya ninayoyasema, na kila mara nimekuwa nikizieleza jamii za aina hizi mbili. Hata hivyo nitatoa mifano mingine.
Bangladesh ni nchi yenye idadi kubwa ya watu (watu zaidi ya milioni 160), na watu wake ni masikini mno. Lakini kwa ujumla ni watu waadilifu, Waislamu wanaofuata mafundisho ya dini yao ya kutochukua kisichokuwa chako na kurejesha ulichoazima na kutendeana haki.
Misingi hii ya uadilifu ndiyo ilimwezesha Muhammad Yunus kufanikisha shughuli za benki ya makabwela inayojulikana duniani kote kama Grameen. Kimsingi benki hii ilianza kwa kutoa mikopo ya kiasi kidogo cha fedha kwa akina mama masikini, hasa wa maeneo ya vijijini.
Ufanisi wa Grameen ulitokana na uaminifu wa wananchi mafukara wanaokopa wakijua kwamba hawana budi kurejesha mkopo ili na  wengine pia wapate fursa ya kukopa. Mara moja inaonekana tofauti kati ya hali hiyo na hali yetu ambayo inatufanya tukope tukijua kwamba hatuna nia ya kulipa mkopo.
Fundisho kubwa tunalolipata kwa Bangladesh ni kwamba si kweli kwamba ulaghai unasababishwa na ufukara kama tunavyoambiwa hapa kwetu wakati mwingine. Nimesikia mara kadhaa watu wakidai eti vitendo vya rushwa vinasababishwa na umasikini wa maofisa wetu. Hii si kweli. Jizi ni jizi tu, hata lingekuwa lina mgodi wa dhahabu. Aidha, tunawajua watu waongofu ambao kipato chao si kikubwa, na bado wanafanya kazi ya umma kwa uadilifu mkubwa.
Sasa tuangalie nini kilitokea miaka kadhaa iliyopita (mwaka 1998) lilipotokea janga la mafuriko yaliyofunika nchi nzima na kusomba nyumba na mali za masikini hawa pamoja na akiba kidogo waliyokuwa wamejiwekea. Nilifanya uchunguzi ili nijue kilichotokea baada ya hapo kwa sababu nilihofu kwamba Grameen ingekufa kwa sababu wateja wake walikuwa wamefanywa kuwa mafukara zaidi. Wapi!
Walilipa. Masharti yalilegezwa kidogo ili kuwapa ahueni katika kulipa, lakini walilipa, na walipolipa na wengine wakapata nafasi ya kukopeshwa. Hiyo benki bado inaendelea na kazi yake njema. Mafanikio yake yanaelezeka kwa neno moja tu: Uaminifu. Sijui kama mambo yamebadilika siku hizi, lakini benki hii ilipoanza haikuwa na makaratasi ya kusaini wala dhamana ya kuweka kama ‘collateral”.
Lakini tuiangalie Bangladesh hiyo hiyo katika sura nyingine, sura ya unyama wa ubepari. Kila mara tumesikia kwamba mamia ya wafanyakazi, hasa wanawake masikini,  wameteketea katika moto uliolipuka kiwandani ambamo walikuwa wamefungiwa.
Wenye mitaji wanawekeza katika viwanda vya nguo ambazo zina soko kubwa katika nchi za Magharibi. Wanaajiri akina mama masikini sana, na malipo yao ni kidogo mno. Kwa kuhofu kwamba wanaweza kuwa wanategea kazi ama wataiba nguo, wanawafungia kwa nje. Unapotokea moto hakuna anayeweza kuchomoka kutoka humo.
Uroho wa faida kubwa inayotokana na kuwanyonya masikini ni chanzo cha mauti na majonzi makubwa. Lakini serikali inashindwa kufanya lo lote kuwadhibiti wenye mitaji hiyo kwa sababu matajiri hao ni maswahiba wakubwa wa wanasiasa. Uswahiba wao si kunywa chai pamoja tu, bali ni uswahiba wa kisiasa kwa sababu matajiri hao ndio wachangiaji wakubwa kwa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi.
Tunaziona hapa sura mbili za nchi moja, na bila shaka zipo nyingine. Katika hizi mbili ninazoziangalia leo, moja ni ya kazi nzuri inayofanywa na benki ya wanyonge, na ambayo msingi wake wa mafaniklo yake ni uaminifu wa watu masikini. Nyingine ni ile ya uroho wa faida walio nao matajiri wenye mitaji iliyowekezwa katika viwanda.
Wanasiasa wanashindwa kuchukua hatua  zinazopasa kwa sababu matajiri ndio waliowaweka madarakani, hata kama wananchi ndio waliopiga kura. Kwa maneno mengine, wanaohusika na vifo vya akina mama hawa si matajiri peke yao bali ni pamoja na wanasiasa wanaofumbia macho vitendo hivyo.
Hebu sasa na  tuichunguze hali yetu. Kwanza, kuhusu uaminifu, hatuna hata haja ya kujilinganisha na Bangladesh. Uaminifu wetu ni sifuri. Kazi ya kumomonyoa maadili na uaminifu wa jamii yetu imefanywa na watawala wetu, tena kwa ustadi mkubwa kana kwamba ndiyo sera inayoongoza nchi yetu hivi sasa.
Nimeandika mara kadhaa kwamba wizi, ulaghai, udanganyifu, ubazazi, unafiki ubabaishaji, undumilakuwili, na kadhalika, haya yote ni sifa mbaya ambazo zinapatikana katika jamii zote za binadamu, na sifa hizi zimekuwapo tangu dunia ilipoanza. Vitabu vitakatifu, ambavyo vimeandikwa zamani kidogo, vimezitaja na kuzilaani sifa hizi.
Kutokana na mafundisho ya vitabu vitakatifu tunatakiwa tuziepuke sifa hizi mbovu, na tuwabaini na kuwatenga, hata kuwapatiliza, wote wenye sifa hizi. Lakini sisi tumezikumbatia, tumezifanya ziwe ndizo sifa za kutupatia viongozi. Tumedharau kabisa mafundisho ya vitabu vitakatifu huku tukijifanya ni Waislamu au Wakristo safi. Hamna kitu!
Kila nikiangalia sioni Muislamu wala Mkiristo. Naona wanafiki watupu.
Lakini mimi sihubiri Uislamu wala Ukristo. Nahubiri usalama wa taifa hili, kama nitakavyoeleza mbele ya safari
-

Jenerali Ulimwengu
src
Raia mwema

0 comments:

Post a Comment

 
Top