SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeitaka Serikali kukusanya kodi kwa watu wenye majumba ya kifahari wanayopangisha watu na taasisi mbalimbali na kulipwa fedha nyingi ikiwemo kwa dola badala ya shilingi.
Pia alitaka Serikali kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa saruji inayoingizwa nchini waliyoiondoa katika bajeti kwani itasababisha saruji zinazozalishwa nchini kukosa soko.
Katibu Mkuu wa TUCTA,Nicholaus Mgaya alisema hayo hivi karibuni wakati akieleza kuwa changamoto alizoizona katika bajeti ya serikali iliyopita wiki hii.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya serikali na kuwezesha fedha kufika kwa wakati katika Halamashauri na wizara mbalimbali kwa ajili ya maendeleo.
Mgaya alisema wachumi wa serikali hawaisaidii serikali kwa kuwa wabunifu katika kuongeza vyanzo vya kipato cha serikali na kubaki na vile vile vya kuongeza bei za soda,bia na sigara.
“Hapa kuna chanzo cha pesa kilicho wazi cha majumba ya kifahari yaliyojengwa katikati ya miji na kupangishwa kwa gharama kubwa mashirika na taasisi nyingine zikilipa kwa dola lakini hawalipi kodi”alisema.
Akizungumzia suala la saruji alisema kuondolewa kwa VAT itasababisha saruji ya ndani kurundikana kama ilivyo sasa kwa sukari na kusababisha watu kukosa ajira.
Pia alishukuru Serikali kufikia asilimia 12 ya kodi na kusema ni sehemu ya kufikia asilimia moja kama walivyoomba na kukanusha taarifa kuwa walikubaliana na serikali kufikia kuwango hicho cha asilimia.

src
Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Top