
NAMSHUKURU Mungu nipo salama, naamini hujambo na unaendelea kupambana kujenga msingi bora wa maisha yako ya baadaye, tafuta utapata, ukikosa usikate tamaa.
Hakuna aliyezaliwa awe masikini, utajiri si kwa ajili ya wachache, maisha bora kwangu na kwako yanawezekana, shida zinavumilika, lakini umasikini haukubaliki.
Pole kama unataabika popote ulipo kwa kutokuwa na kipato cha uhakika, usijichukie, usiyachukie maisha, jipe moyo kwamba ipo siku na wewe hutajiuliza utapata vipi fedha, ila utachagua uzitumie vipi, wapi na ikiwezekana na nani.
Kama huna ajira tambua kwamba, wewe ni miongoni mwa mamilioni ya Watanzania hasa vijana wanaohangaika kutafuta kazi kila inapoitwa leo. Kuna vijana wenye ujuzi wa fani mbalimbali lakini hadi sasa ugumu wa maisha umekuwa sehemu ya maisha yao.
Wapo pia ‘waliopikwa’ kinadharia zaidi, wamehitimu shule za msingi, sekondari na hata vyuo lakini kwa kuwa waliandaliwa kuomba ajira, bado ni tegemezi, wametuma maombi hadi wamechoka, maisha mazuri kwao ni msamiati.
Wengi wakiwemo wanasiasa, viongozi wa Serikali, wasomi na watu wa kada tofauti wanazungumzia umasikini na ukubwa wa tatizo la ajira lakini hawasemi kuwa kiini cha tatizo ni mfumo wa elimu nchini.
Namshangaa anayesema vijana wanachagua kazi, bila yeye kuchagua kazi angekuwa anafanya kazi anayoifanya? Hoja hapa si kijana kuchagua kazi, ila ni kwa namna gani anawezeshwa kuimudu hiyo kazi aliyoichagua.
Suala la kuchagua kazi haliepukiki na ndiyo maana watu wana ndoto zao, na hata shuleni au vyuoni kuna fani tofauti. Viongozi na jamii kwa ujumla wasikwepe tatizo la msingi linalosababisha wananchi wengi wasiwe na ajira.
Suluhisho la tatizo la ajira lazima lianzie kwenye mitaala, Watanzania kwa ujumla hawawezi kukombolewa kwa ongezeko la madarasa, maabara na nyumba za walimu.
Mfumo wa elimu yetu unawaandaa wahitimu waajiriwe, lakini uchache wa fursa za kuajiriwa na hali halisi ya maisha wanalazimika kujiajiri hasa kuwa wajasiriamali.
Mfumo wa sasa uchumi ni wa kibepari, suala la biashara halikwepeki, mtaala wa elimu Tanzania umelizingatia hilo?
Vijana wanaambiwa wachangamkie fursa za kujiongezea kipato , lakini hao wanaosema hivyo wanajifanya hawajui kuwa, mitaala ya shule za msingi na hata sekondari haiwaandai wahitimu kuwa wajasiriamali, au wawekezaji.
Leo mhitimu wa darasa la saba analazimika kuwa mchuuzi wa bidhaa lakini shuleni hakufundishwa chochote kuhusu namna bora ya kufanya biashara, ubunifu wa biashara, namna ya kupata mtaji na masoko, kanuni za kufanya biashara katika mazingira ya ushindani, umuhimu ubunifu, kuthubutu, kutafiti masoko ndani na nje ya nchi, kufanya biashara kwa mtandao, namna ya kuongeza wigo wa mtaji nk. Siku njema. bmsongo(at)hotmail.com
0 comments:
Post a Comment