Licha ya vijana hao, lakini pia kuna kundi lingine la vijana ambao wanahitimu elimu ya sekondri, vyuo vya ufundi na shule ya msingi, nao wanaingia mitaani kusaka ajira huku wakiwa hawana uwezo wowote.
Kuwepo kwa vijana wengi nchini bila kuwa ajira, limekuwa linazungumzwa na wadau mbalimbali kuwa ni bomu ambalo linasubiri kulipuka.
Ndio maana watu 20,000 wenye shahada ya kwanza wanajitokeza kuomba nafasi 70 tu za maofisa wa uhamiaji, jambo ambalo limewashtua wengi na kuthibitisha kuwa ni kweli kuna atizo la ajira.
Kitendo cha Uhamiaji kuwapeleka vijana 10,000 ambao walichukuliwa kufanya usaili na kuwapeleka Uwanja wa Taifa, hili liliithibitishia umma wa Watanzania kwamba ni kweli tatizo la ajira ni bomu.
Ni bomu kwa sababu vijana ambao hawana ajira ni rahisi kushawishiwa na kujiingiza kwenye vitendo viovu. Makundi hatari kama ya Boko Haram, Al qaeda na Al Shabaab wamefanikiwa kujenga mitandao yao kwa kutumia vijana wasomi, ambao hawana ajira.
Lakini, jambo la kutia moyo ni kwamba wafanyabiashara, wasomi baadhi wamekuwa wanatoa mwito kuwataka vijana wasilemae kusubiri ajira za maofisini, badala yake waangalie fursa zilizopo nchini ili ziwasaidie kuwapatia kipato na wasijikute wanajiingiza kwenye makundi hatari ya uhalifu.
Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wanashauri vijana kufumbua macho na kuziona fursa zilizopo na kuzichangamkia. Mwito huo pia umerudiwa juzi na bosi wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi, Filbert Rweyemamu kwenye semina ya ‘Tufanikiwe Pamoja’.
Semina hiyo ilikuwa na lengo la kuwahamasisha wakazi wa Kahama, wakiwemo wajasiriamali wadogo, kuchangamkia fursa zilizopo kwenye maeneo yao, ambazo zinaweza kuwapatia vipato au kuwanyanyua vipato vyao.
Binafsi, naunga mkono wa watu wenye mtazamo huo, kuwa umefika wakati vijana waache kulalamikia kuwa hawana ajira, huku wakishinda vijiweni, badala yake waangalie namna gani wanaweza kujishughulisha ili waweze kujiondoa kwenye lindi la umaskini.
Tutambue kuwa Mungu ametoa saa 24 kwa maskini, matajiri na wasomi, hivyo fursa pekee ni kutumia akili, viungo na nguvu ulizonazo kuhakikisha kuwa unajishughulisha kikamilifu ili kutimiza ndoto zako.
Naamini kuwa hakuna mtu aliyezaliwa tajiri, na matajiri wa leo sio waajiriwa, bali ni wajasiriamali ambao waliziona fursa zilizopo na wakazichangamkia vizuri na leo hii wamefikia hapo walipo. Kwenye ajira hakuna utajiri, bali ni kupata pesa ya kujikimu tu.
Ndio maana naamini iwapo vijana watafumbua macho na kuangalia fursa zilizopo kwenye maeneo yao, wataweza kupunguza tatizo la ajira.
Mfano, kama kwenye eneo lako unaloishi, kuna watu wanahitaji vitafunwa vya chai na vinavyopatikana vinapikwa kwenye njia ya asili, kwa nini usiboreshe fursa hiyo?
Kama kwenye eneo lako, kuna walaji wazuri wa samaki wa kukaanga na upatikanaji wake ni ule ule wa kukaanga na kuweka hadharani, huku inzi wakishangilia kuwepo kwa samaki hao, kwa nini kijana usiichukue hiyo fursa na kuiboresha zaidi ili uvutie wateja wengi?
Kama eneo lako ni la kilimo na bei za mazao zinazidi kudidimia, kwa nini tusibadilishe mfumo wa kilimo tukaenda kulima miti ya mbao, kwa vile kila kukicha mahitaji ya mbao ni makubwa?
Hivyo kitendo cha kulalamika kuwa hakuna ajira ni sawa, lakini naamini kwamba umefika wakati Serikali yetu kwa kushirikiana na wadau wengine, ikiwemo sekta binafsi na shirika la uwezeshaji la taifa, kuhakikisha kuwa linawafunda vijana ili wamalizapo masomo, wawe na macho makali ya kuziona fursa zilizopo.
Haiwezekani vijana wote wanaohitimu vyuo vikuu na wale wanaohitimu sekondari, wapate ajira rasmi. Ni lazima tuangalie maeneo mengine ya kuwasaidia vijana wetu, maana eneo la kilimo linazidi kudidimia; huku mapinduzi ya viwanda ambayo yanategemewa na nchi nyingi kutoa ajira kwa vijana, hapa kwetu hakuna dalili za kuwepo mapinduzi.
src
Habari Leo
0 comments:
Post a Comment