Mwandishi, mwigizaji na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Vitabu nchini (UWAVITA), Edwin Semzaba  

Unapotaja majina kumi ya waandishi mahiri wa vitabu nchini, jina la Edwin Semzaba haliwezi kukosekana.
Huyu ni mwandishi, mwigizaji na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia ni mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Vitabu nchini (UWAVITA).
Kitabu chake cha Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe, ni miongoni mwa vitabu vilivyompatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kikiwa miongoni mwa vitabu vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili kama kitabu cha kiada kwa shule za sekondari, kitabu cha Ngoswe kwa kiasi kikubwa kimekuwa na mchango katika kujenga fasihi ya Mtanzania.
Mwandishi wetu Maimuna Kubegeya alifanya mahojiano naye hivi karibuni kuhusu maisha yake kama mtunzi na msanii.
Swali: Ni lini hasa ulinza kazi ya uandishi na nini hasa kilikuvutia kuingia kwenye tasnia hiyo?
Semzaba: Nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana kusoma vitabu. Hii ilitokana na ukweli kuwa baba na mama yangu walikuwa walimu hivyo, nyumbani kwetu kulikuwa na vitabu vingi vya hadithi.
Jambo hili lilichangia kunihamasisha kupenda kusoma. Hivyo hadi nafika darasa la nne nilijikuta nina uwezo wa kuandika hadithi fupi na mashairi. Darasa la tano niliweza kuandika barua kwa Kiingereza.
Wakati naingia darasa la saba nilikuwa na uwezo mkubwa wa kuandika na kupangilia maneno.
Swali: Unakumbuka ni vitabu gani ulianza kusoma
Semzaba: Hadithi ya Alan Quatermain (Msolopagazi), Mashimo ya Mfalme Suleimani, Alfu Lela Ulela ni miongoni mwa vitabu vya mwanzo nilivyowahi kusoma.
Hivi vilikuwa vikitumika shuleni lakini kwa kuwa vilikuwa vikiugusia ujio wa mtu mweupe Afrika baadaye viliondolewa
Swali: Tueleze ilivyokuwa hadi ukaandika kitabu cha Ngoswe

Semzaba: Niliandika kitabu cha Ngoswe nikiwa kidato cha pili, wakati huo nilikuwa na miaka 16 tu.

Tena ilikuwa ni kwa sababu ya kukimbia somo la hesabu hivyo wakati najificha nilitumia muda huo kuandika. Nilibadilisha tu mhusika mkuu akawa mtu mzima na siyo mwanafunzi.

Hii ilikuwa mwaka 1967 wakati wa sensa ya kwanza kabisa ya watu ya kufanyika nchini. Enzi hizo nilikuwa mwanafunzi wa Livingstone College, sasa Sekondari ya Kigoma.

Nikiwa miongoni mwa wanafunzi waliochaguliwa kufanya sensa hiyo, nilipata wasaa wa kusoma mazingira niliyokuwa nikifanyia kazi na huko ndipo wazo la kuandika Ngoswe liliponijia.

Uandishi wake niliuanza baada ya kurudi shule. Hata hivyo kilikuja kuchapishwa miaka ishirini baadaye baada ya kuigizwa sana hapa nchini na Kenya.

Swali: Kipi kilisukuma mchakato wa kukichapisha baada ya muda huo wote
kupita?
Semzaba: Kwanza ule mchezo nilipokuja hapa chuoni ulichapishwa na kuwekwa katika shubaka ofisini. Akaja mwalimu mmoja wa Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Thomas Chang’a, akawa anataka mchezo wa kuigiza.

Alipousoma akasema huu ni mzuri. Hivyo akaupeleka Redio Tanzania kuchezwa ama sivyo usingepata nafasi ya kuchapishwa. Kwani baada ya hapo ndiyo ulipata fursa ya kuchapishwa.

Hata hivyo, wakati kitabu hicho kinatoka, Chang’a ambaye aliigiza kama Ngoswe, alikuwa ameshafariki huko Uingereza alikokwenda kwa ajili ya masomo.

Mwingine aliyetoa mchango mkubwa ni Elly Siagi ambaye kwenye mchezo wa redio alicheza kama Jaluo na ofisa wa sensa

Swali: Nini hasa maana ya neno Ngoswe na kwa nini ulikiita jina hilo?
Semzaba: Kimsingi jina la Ngoswe lilikuwa jina langu la jukwaani.

Neno hilo linamaanisha panya kwa Kibondei. Nilijipachika jina hilo kwa kuwa tu niliona kama linachekesha, hivyo nilipotunga kitabu nikaona nilitumie.

Kingine ni kwamba, kile kitabu sikukiita Ngoswe, bali nilikiita Hesabu Iliyoharibika.

Sasa ili uvutie uliporushwa redioni wakaupa jina Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe.

Swali : Unafaidikaje na kazi yako hii ya Ngoswe?

Semzaba: Ni vigumu sana kufaidika na kazi ya uandishi hapa nchini.

Licha ya kutumika shuleni, huwezi kuamini napata faida kidogo sana kutokana na ukweli kuwa wako watu wanadurufu kazi yangu na kuiuza kwa manufaa yao.

Jambo hili pia limesababisha kubadilika badilika kwa muonekano wa kitabu hicho.

Tangu kuchapishwa kwake mara ya kwanza nimebadilisha wachapishaji karibu mara tatu sasa.
Swali: Unakabiliana na changamoto gani katika kazi yako hii ya uandishi?

Semzaba: Changamoto kubwa inayonikabili ukiachilia mbali suala la hati miliki, ni matumizi makubwa ya vyombo vya habari vya kielektroniki. Kutokana na uwepo wa mitandao ya inteneti, watu sasa hawasomi vitabu.

Katika hili naweza kusema hata magazeti pia yanachangia. Watanzania wengi wanapenda habari fupi sasa linapokuja suala la kusoma habari ndefu ni mtihani.
Swali: Ukiachilia mbali kitabu cha Ngoswe, una kazi nyingine?

Semzaba: Nimeandika vitabu vingi. Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na Tendehogo, (1982), Sofia wa Gongo la Mboto (1985), Mkokoteni (1988), Tausi wa Alfajiri (1996), Funke Bugebuge (1999) , Tamaa ya Boimanda (2002), na Marimba ya Majaliwa (2008).

Swali : Wizi wa kazi za wasanii ni tatizo sugu, ni nini mtazamo wako katika hili?

Semzaba: Ni kweli kabisa na Serikali kutotilia mkazo suala la uangalizi na udhibiti wa kazi za wasanii. Tumekuwa tukiibiwa kwa siri na kwa dhahiri.

Chukulia mfano kitabu changu hiki cha Ngoswe kimechapiswa kwa zaidi ya miongo miwili sasa, lakini ukweli ni kwamba mapato ninayopata hayalingani na kazi yangu. Hapa utaona ni kwa jinsi gani haki ya msanii inavyopotea.

Swali: Kuna tetesi kuwa uliwahi kuwa mwanamasumbwi, Je, kuna uweli wowote.

Semzaba: Ndio niliwahi kuwa mpiganaji mahiri katika mchezo wa masumbwi. Nilianza kucheza mchezo huo nikiwa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Kimsingi mchezo wa ngumi ndio mchezo ninao upenda zaidi. Nakumbuka kipindi kile niliwahi kushinda katika mashindano ya Vyuo Vikuu vya Afrika ya Mashariki karibu mara tatu mfululizo.

Mipango yangu ilikuwa ni kuwa mwamasumbwi wa kimataifa, lakini ndoto yangu ilizimwa na ugonjwa wa macho.

Swali: Nini matarajio yako ya baadaye?

Semzaba: Matarajio yangu ya baadaye kwanza ni kufanya sehemu ya pili ya Ngoswe.

Sehemu hii ya pili itafahamika kwa jina la Ngoswe karudi. Lakini pia natarajia kuendeleza kampuni yangu ya uchapishaji inayofahamika kama Exodia Publishers.

0 comments:

Post a Comment

 
Top