WATAALAMU wa masuala ya ebola, wamehoji ni kwa nini wafanyakazi wa afya wa Marekani, ndio tu wanaopewa dawa za majaribio. Wataalamu watatu wa masuala hayo, wametaka dawa hizo za majaribio na chanjo, zipewe kwa watu wa Afrika Magharibi, ambako kuna mlipuko wa ugonjwa huo hatari.
Kwa sasa ugonjwa huo umesambaa katika nchi tatu za ukanda huo. Wafanyakazi watatu wa afya kutoka Marekani, waliopata maambukizi ya ugonjwa huo nchini Liberia, walipewa dawa ambayo haijapitishwa kisha wakaondolewa na kupelekwa Marekani.
Wataalamu hao, akiwemo Peter Piot, aliyegundua ebola mwaka 1976, walisema waafrika walioathirika na ugonjwa huo, wanatakiwa kupewa fursa kama walizopewa Wamarekani hao.
Piot, David Heymann na Jeremy Farrar ambao ni maprofesa wa magonjwa ya kuambukiza wenye ushawishi mkubwa na wakurugenzi wa Shule ya London ya Elimusiha na Dawa za Tropiki, Kituo cha Chatham kinachojishughulisha na Usalama wa Afya Duniani na Mfuko wa Welcome, walisema kuna utafiti unafanyika wa dawa na chanjo ambazo zinaweza kutumika kutibu ebola.
"Serikali za Afrika zinapaswa kuruhusiwa kufanya maamuzi iwapo zitumie au zisitumie bidhaa hizo…mfano kulinda na kutibu wafanyakazi wake wa afya ambao wako katika hatari ya kupata maambukizi,” ilisema taarifa yao ya pamoja.
Walisema Shirika la Afya Duniani (WHO) linapaswa kuruhusu majaribio ya tiba hiyo.
Karibu watu 900 wa nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia wamekufa kwa ebola. Wengine zaidi ya 1,600 wamepata maambukizi tangu ugonjwa huo ulipoanza Guinea mwezi Februari.
Wafanyakazi wawili wa afya wa Marekani, ambao walipata maambukizi ya ebola wakiwa Liberia, waliona afya zao zikiimarika kwa kiasi kikubwa wakiwa nchini humo baada ya kupewa dawa hizo za majaribio zinazoiwa ZMapp.
Dawa hizo zimeboreshwa na kampuni binafsi ya Mapp Biopharmaceutical, yenye makazi yake mjini San Diego, Marekani.
Wakati huo huo, WHO litaitisha mkutano wa siku mbili wa kamati yake ya dharura kujadili mlipuko wa ebola.
Kwa mujibu wa WHO, hadi sasa watu 1,603 wameambukizwa ugonjwa huo, ambapo 887 wamefariki dunia. Ugonjwa huo umesababisha vifo nchini Guinea, Liberia, Nigeria na Sierra Leone. Waliokufa kutokana na ugonjwa huo nchini Liberia, wamefikia 268 ikiwa ni pamoja na wauguzi 37.
Kwa sasa wauguzi wametelekeza vituo vyao vya kazi. Kila siku mwili wa mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo, huokotwa mtaani. Nchini Sierra Leone amri ya kutotoka nyumbani kwa siku nzima iliwekwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Freetown, hivyo kusababisha maduka na ofisi zote kufungwa ili kukagua hali ya maambukizi.
Nchini Marekani, daktari wa pili aliyeambukizwa ebola akitokea Afrika Magharibi, aliwasili nchini humo na kuanza kupatibiwa
0 comments:
Post a Comment